Psalms 27

Sala Ya Kusifu

(Zaburi Ya Daudi)


1 a Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
nimhofu nani?

2 bWaovu watakaposogea dhidi yangu
ili wanile nyama yangu,
adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia,
watajikwaa na kuanguka.

3 cHata jeshi linizunguke pande zote,
moyo wangu hautaogopa;
hata vita vitokee dhidi yangu,
hata hapo nitakuwa na ujasiri.


4 dJambo moja ninamwomba Bwana,
hili ndilo ninalolitafuta:
niweze kukaa nyumbani mwa Bwana
siku zote za maisha yangu,
niutazame uzuri wa Bwana
na kumtafuta hekaluni mwake.

5 eKwa kuwa siku ya shida,
atanihifadhi salama katika maskani yake,
atanificha uvulini mwa hema yake
na kuniweka juu kwenye mwamba.

6 fKisha kichwa changu kitainuliwa
juu ya adui zangu wanaonizunguka.
Katika maskani yake nitatoa dhabihu kwa kelele za shangwe;
nitamwimbia Bwana na kumsifu.


7 gIsikie sauti yangu nikuitapo, Ee Bwana,
unihurumie na unijibu.

8 hMoyo wangu unasema kuhusu wewe,
“Utafute uso wake!”
Uso wako, Bwana “Nitautafuta.”

9 iUsinifiche uso wako,
usimkatae mtumishi wako kwa hasira;
wewe umekuwa msaada wangu.
Usinikatae wala usiniache,
Ee Mungu Mwokozi wangu.

10 Hata kama baba yangu na mama wakiniacha,
Bwana atanipokea.

11 jNifundishe njia yako, Ee Bwana,
niongoze katika njia iliyonyooka
kwa sababu ya watesi wangu.

12 kUsiniachilie kwa nia za adui zangu,
kwa maana mashahidi wa uongo
wameinuka dhidi yangu,
wakipumua ujeuri.


13 lNami bado nina tumaini hili:
nitauona wema wa Bwana
katika nchi ya walio hai.

14 mMngojee Bwana,
uwe hodari na mwenye moyo mkuu,
nawe, umngojee Bwana.
Copyright information for SwhKC